Thursday, October 13, 2016

MAGUFULI ATUMBUA JIPU LINGINE.


Hatua ya Rais John Magufuli kuzuia viongozi waandamizi wa mikoa na wilaya kuhudhuria kilele cha Mbio za Mwenge mkoani Simiyu, imeokoa Sh1.2 bilioni ambazo zingetumika kulipia posho na usafiri.

Wakuu wa mikoa 30, wa wilaya 161, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri na mameya, wasaidizi wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, waratibu wa Mwenge wa wilaya na mikoa pamoja na madereva wa viongozi wote hao wangehudhuria sherehe hizo na wangeigharimu Serikali kiasi hicho cha fedha.

Kwa makadirio, wakuu wa mikoa 30 kila mmoja angelipwa posho ya kila siku Sh120,000 kwa siku saba, msaidizi wake Sh80,000 kwa siku na dereva Sh50,000. Katibu tawala angelipwa Sh120,000 kwa siku na dereva wake Sh50,000 wote kwa siku hizo saba.

Wakuu wa wilaya 161 wangelipwa posho ya Sh120,000 kwa siku kwa muda huo na madereva wao Sh50,000.

Katika msafara huo wangekuwapo makatibu tawala wilaya 161 ambao nao wangelipwa posho ya Sh120,000 na madereva wao Sh50,000 kila siku.

Wakurugenzi wa halmashauri 161, wenyeviti na mameya wangelipwa Sh120,000 kwa siku. Madereva wao kila mmoja angepokea posho ya Sh50,000 kila siku kwa muda wa siku saba.
Wengine ambao wangehudhuria sherehe hizo ni waratibu wa Mbio za Mwenge wa mikoa na wilaya ambao walitarajiwa kulipwa posho ya Sh80,000 kila mmoja.


Tofauti na posho hizo, waratibu hao pia wangelipwa nauli za kwenda na kurudi kutoka katika maeneo yao ya kazi na viongozi wengine wa juu wangepewa posho za kununulia mafuta.

No comments: