MAREHEMU DIDAS MASABURI.
Rais John Magufuli ameitumia salamu za rambirambi familia ya Meya Mstaafu wa
Jiji la Dar es Salaam Dkt. Didas Masaburi aliyefariki dunia jana katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya Ikulu jijini Dar es Salaam imesema katika salamu hizo Rais
Magufuli amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dkt. Masaburi kwa mshituko na
masikitiko makubwa na kwamba anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na
marafiki katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.
"Poleni sana familia ya Dkt. Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu sana
kwenu, lakini niwahakikishie kuwa sote tumeguswa sana na msiba huu kwa kuwa
tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa kwa moyo wake
wote na aliyesimamia kile alichokiamini" amesema Rais Magufuli katika salamu
hizo.
Aidha, Magufuli amewapa pole wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ambao wamempoteza Mwana CCM mwenzao pamoja na Viongozi na watumishi wa
Jiji la Dar es Salaam ambao walifanya nae kazi alipokuwa Meya wa Jiji.
Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.
"Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina" amemalizia Rais
Magufuli.
No comments:
Post a Comment