DK. OTHMAN KILOLOMA.
TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa mara ya kwanza imefanya
upasuaji mkubwa kwa mafanikio wa kunyoosha mfupa wa mgongo wa mtoto wa miaka 13
uliokuwa umepinda (kibiongo).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Othman Kiloloma amesema jana jijini Dar
es Salaam alipokuwa akielezea upasuaji huo uliofanyika kwa saa tano.
Dk Kiloloma amewaeleza waandishi wa habari kuwa, upasuaji huo umefanyika kwa
kutumia teknolojia ijulikanayo kama ‘posterior instrumentation and fusion’
ambayo inahusisha uwekaji wa vyuma maalumu kwenye mfupa wa mgongo katika sehemu
ya juu na chini ya mfupa wa mgongo na kuufanya unyooke kama inavyotakiwa.
“Taasisi ya MOI imefanikiwa kufanya upasuaji huo kwa kupitia madaktari bingwa
walioko kwenye mafunzo ya ubobezi wa juu katika upasuaji wa mifupa na mgongo kwa
watoto kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Marekani,” alisema Dk
Kiloloma.
Alisema uanzishwaji wa upasuaji huo umetokana na kuanzisha kwa ushirikiano wa
kimafunzo kati ya Taasisi ya MOI na Chuo cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji cha
Afrika Mashariki, Kati na Kusini (COSECSA) na madaktari bingwa kutoka
Marekani.
Mkurugenzi huyo alisema uanzishwaji wa upasuaji huo wa kunyoosha migongo ya
watoto iliyopinda, unatarajiwa kuisaidia serikali kupunguza rufaa za kuwapeleka
wagonjwa nje ya nchi ambazo ni za gharama kubwa.
“Watoto hao waliokuwa wanaenda India na sehemu nyingine, iligharimu dola 60,”
alisema.
No comments:
Post a Comment