Mgombea urais wa chama cha Democratic Donald Trump amesema mpango wa mpinzani wake Hillary Clinton kuhusu kutatua mzozo Syria utaanzisha "Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia".
Amesema Marekani inafaa kuangazia zaidi kushinda vita dhidi ya kundi linalojiita Islamic State badala ya kulenga kumshawishi au kumshinikiza Rais wa Syria Bashar al-Assad kung'atuka uongozini.
Bi Clinton amekuwa akipendekeza kutolewe marufuku ya ndege kutopaa katika anga ya Syria, mpango ambao baadhi wanasema huenda ukasababisha mgogoro na ndege za kivita za Urusi ambazo zinatekeleza mashambulio dhidi ya waasi wanaompinga Bw Assad.
Maafisa wa kampeni wa Bi Clinton wamemtuhumu Bw Trump kwa "kuwachezea Wamarekani kupitia wasiwasi wao".
Bw Trump pia amewashambulia wafuasi na viongozi wa Republican ambao wamekataa kumuunga mkono.
"Iwapo tungekuwa na umoja, hatungeshindwa na Hillary Clinton kwenye uchaguzi huu," aliambia shirika la habari la Reuters katika uwanja wa gofu wa Trump National Doral mjini Miami, Florida.
Mgombea huyo ametishia kwamba hali mbaya zaidi itatokea iwapo mpango wa mpinzani wake wa chama cha Democratic wa kutaka kudhibiti anga ya Syria utatekelezwa.
"Mtajipata katika Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia huko Syria iwapo tutamsikiliza Hillary Clinton," Bw Trump amesema.
"Hampigani tena dhidi ya Syria, mnapigana na Syria, Urusi na Iran, mnafahamu?
"Urusi ni taifa lenye uwezo wa kinyuklia, lakini taifa ambalo silaha zake za nyuklia hufanya kazi kinyume na nchi nyingine ambazo kwao ni maneno tu."
Amedokeza kuwa Bi Clinton hataweza kufanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin ikizingatiwa kwamba amekuwa akimshutumu sana kiongozi huyo kwenye kampeni.
Bw Trump ameshangaa: "Ataenda vipi na kufanya mazungumzo na mtu ambaye amemuonyesha kuwa ni mtu mwovu sana?" iwapo atachaguliwa kuwa rais tarehe 8 Novemba.
Maafisa wa kampeni wa Bi Clinton hata hivyo wamepuuzilia mbali ukosoaji huo na kusema wataalamu wa usalama wa taifa wa Republican na Democratic wamemshutumu Bw Trump na kusema hafai kuwa amiri jeshi mkuu.
"Kwa mara nyingine, anazungumza kama kasuku kumhusu Putin na kuchezea wasiwasi wa Wamarekani, lakini anakataa kusema mipango yake ya kuwashinda ISIS au kumaliza mzozo wa kibinadamu nchini Syria," msemaji wa Bi Clinton, Jesse Lehrich amesema kupitia taarifa.
'Kuua watu wa Syria'
Tahadhari hiyo kutoka kwa Bw Trump ni sawa na tahadhari iliyotolewa na afisa mkuu wa jeshi la Marekani katika kikao cha wabunge.
Mwenyekiri wa majeshi ya pamoja Jenerali Joseph Dunford aliambia wabunge kuwa kutangaza marufuku ya kuzuia ndege kupaa anga ya Syria kunaweza kusababishwa vita na Syria.
"Kwa sasa, seneta, ndipo tuweze kudhibiti anga yote ya Syria, itatuhitaji kwenda vitani na Syria na Urusi," Jenerali Dunford aliambia kamati ya huduma za jeshi katika seneti.
"Huo bila shaka ni uamuzi ambao sitachukua."
Kwenye mdahalo wa mwisho wa urais Nevada 20 Oktoba, Bi Clinton alieleza uungaji mkono wake kwa hatua hiyo.
"Marufuku ya ndege kutopaa inaweza kuokoa maisha na kuharakisha mwisho wa mzozo huo," alisema.
Lakini mwaka 2013, kwenye hotuba kikao cha Goldman Sachs, Bi Clinton alikuwa amesema marufuku kama hiyo inaweza "kuwaua watu wengi wa Syria", kwa mujibu wa maandishi ya hotuba hiyo yaliyofichuliwa na Wikileaks.
Vifo vya raia vinaweza kutokana na haja ya wanajeshi wa Marekani kushambulia ngome za wanajeshi wa Syria ambazo zimo maeneo yenye raia wengi.
Nini kinafuata?
Wagombea wanatarajiwa kutumia siku 14 zilizosalia kujipigia debe. Wanatarajiwa kupiga kampeni sana majimbo yanayoshindaniwa kama vile Ohio, Carolina Kaskazini, Florida na Pennsylvania
Uchaguzi utafanyika Jumanne 8 Novemba kuamua Rais wa 45 wa Marekani.
Rais mpya ataapishwa 20 Januari 2017
No comments:
Post a Comment