Serikali iko katika mkakati wa kuwabana wanafunzi wanaopewa mikopo katika fani za kipaumbele, kutumikia katika utumishi wa umma nchini kwa muda fulani ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuwapa kipaumbele inatimia.
Fani hizo ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta, gesi asilia, sayansi asilia, mabadiliko ya tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Hatua hiyo inatokana na serikali kubaini kuwapo wanafunzi wanaosomea fani hizo ili kupata mikopo, lakini baada ya kumaliza hukimbilia kufanya kazi nyingine au nje ya nchi, hivyo upungufu wa wataalamu waliowakusudia kubaki kama ilivyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya aliyasema hayo hivi karibuni, alipozungumzia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Alieleza kuwa serikali inafikiria kuwe na utaratibu kwa wanaonufaika na mikopo ya kipaumbele kuingia makubaliano na serikali.
Manyanya alisema kuja na mtazamo na makubaliano hayo, yatakuwa kutumikia katika fani hiyo kwa kipindi fulani; na anapotoka aruhusiwe kwani sasa wapo wanapopangiwa huripoti na kuondoka bila kufanya kazi hizo.
Alisema suala hilo halitakuwa jipya kwani hapo nyuma walikuwa wakibanwa kuwa lazima kufanya kazi angalau kwa miaka mitano serikalini na baadaye ni ruhusa kwenda popote, lakini kwa sasa hawawezi kuwabana wote, lakini lazima kufanya hivyo kwa hao wa kipaumbele.
Alitoa onyo kwa wanafunzi wanaosomea masomo hayo ya kipaumbele, kama hawana wito wa kufanya kazi hizo kuacha.
Alitoa mfano wa walimu wa sayansi ambao serikali inatoa fedha ili kusaidia wanafunzi katika shule za wananchi hususan vijijini, ambako hakuna walimu wa sayansi, hesabu na mengineyo.
Aliwaasa wanafunzi hao kuwa kama nia yao ni kupata mikopo tu, pesa hizo siyo nzuri kwao kwa sasa.
Akizungumzia ulipaji mikopo hiyo, Manyanya alisema wanaboresha sheria ya kukusanya madeni kwa kushirikiana na waajiri.
Alisema serikali itakusanya madeni hata kwa wakopaji ambao wamejiajiri kwa sababu wengi wakimaliza masomo hawafikirii kulipa.
Alisema sasa lazima, wakopaji watambue fedha hizo ni mikopo na lazima kulipa. Alisema kwa wakopaji watakaoajiriwa, wizara inataka mikopo huo kuwa wa kwanza kukatwa kabla ya mingine ili kuepuka kuingiliana na sheria za kazi, zinazotaka mkopaji kuachiwa fedha fulani katika mshahara wake.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hosteli katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais John Magufuli alisema hadi sasa serikali inadai Sh trilioni 2.6 ambazo zilikopeshwa kwa wanufaika mbalimbali wa elimu ya juu, lakini hadi sasa hawajarejesha na hiyo inaleta changamoto kwa waombaji wapya.
No comments:
Post a Comment