Monday, October 24, 2016

MFALME WA MOROCCO AMEWASILI NCHINI NA KITANDA NA MAZULIA YA KIFALME.

Rais John Magufuli akiwa na Mfalme wa Morocco,

 Mfalme Mohammed VI wa Morocco amewasili nchini akiwa na msafara wa ndege tano zilizobeba vifaa vyake, ikiwamo kitanda na mazulia ya kifalme.
Mfalme Mohammed aliwasili jana saa 11:15 jioni akiwa na ujumbe wake wa watu zaidi ya 150, wakitokea nchini Rwanda.
Kabla ya kuwasili kwa ndege yake, zilitangulia ndege mbili ndogo za Morocco zilizokuwa na ujumbe ulioambatana naye.
Awali, Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga alinukuliwa akisema msafara wa Mfalme huyo ulitanguliwa na ndege mbili zilizobeba vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi yake kwa kipindi chote atakachokuwapo nchini.
“Nadhani mnajua mapokezi ya kifalme yalivyo, wenzetu wanapenda kuandaa wenyewe kila kitu atakachotumia mfalme wao. Ndege mbili zimewasili zikiwa zimebeba vifaa mbalimbali vikiwamo kitanda na mazulia ya kifalme,” alisema Dk Mahiga kabla ya ujio wa Mfalme Mohammed VI.
Mfalme Mohamed VI alipokewa uwanja wa ndege na vikundi mbalimbali vya burudani na raia wa Morocco wanaoishi nchini. Ulinzi uliimarishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wa maofisa usalama wa pande zote mbili kwa kuzunguka pande zote za uwanja huo.
Mfalme huyo aliambatana na vyombo vya habari, ikiwamo televisheni maalumu ya familia ya kifalme na televisheni ya Taifa ya Morocco. Kamera za vyombo vya habari vya Morocco na Tanzania zilitawanywa sehemu mbalimbali za uwanja huo ili kupata matangazo ya tukio hilo moja kwa moja.
Baadhi ya wananchi kusimama kando ya barabarani kushuhudia msafara wa kiongozi huyo wa Morocco ulipokuwa ukipita kutokea uwanja wa ndege, walikuwa wakishangilia huku wakipunga mikono.
Kilichomleta  Mfalme Tanzania
Mfalme huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mambo yatakayojadiliwa na viongozi hao ni uhusiano baina ya nchi zao na Morocco kutafuta uungwaji mkono ili irejee kwenye Umoja wa Afrika (AU).
Mfalme huyo atafanya ziara rasmi ya siku tatu na baadaye ataanza likizo yake na kutumia siku tano zaidi kutembelea vivutio vya utalii.
Serikali za Tanzania na Morocco zitatiliana saini makubaliano mbalimbali ya kibiashara ikiwa ni moja ya mkakati wa nchi hizo kuimarisha uchumi.
Waziri Mahiga alisema lengo la ziara hiyo ni kuanzisha diplomasia ya kiuchumi kwa kuwa Morocco ni moja ya nchi za Afrika zenye maendeleo.
Alisema uhusiano wa Tanzania na Morocco ulianza siku nyingi kupitia ubalozi wa Tanzania uliopo Ufaransa na Ubalozi wa Morocco nchini Kenya. Alisema Serikali ya Morocco imeonyesha nia ya kuanzisha ubalozi wake nchini.
Akizungumzia zaidi kuhusu ujio wa Mfalme huyo, Dk Mahiga alisema Tanzania na Morocco zitatiliana saini mikataba zaidi ya 16 ambayo baadhi yake itakuwa kati ya Serikali Kuu, taasisi na mashirika.
“Hii ni ziara ya kipekee kwa sababu ndiyo mara ya kwanza kwa Mfalme kutembea hapa nchini. Mfalme Mohammed VI ataambatana na wajumbe zaidi ya 150 ambao wengi wao wanatoka familia ya kifalme,” alisema Dk Mahiga.
Waziri huyo alisema ajenda nyingine ya ziara hiyo ni Morocco kuomba kuungwa mkono na Tanzania juu ya azima yake ya kutaka kurejea AU tangu ilipojitoa miaka 32 iliyopita.
Alisema Tanzania inaunga mkono dhamira ya Morocco kurejea AU kwa sababu ni moja ya nchi za Afrika na inahitaji kushirikiana kupitia umoja huo.
Alisema sababu ya Morocco kujitoa kwenye umoja huo ilikuwa ni mgogoro kati ya nchi hiyo na Sahara Magharibi.
“Wao wameona ni fursa kurejea katika Umoja wa Afrika, na sisi hatuoni tatizo katika hilo kwa sababu tunahitaji kushirikiana. Licha ya kutokuwa katika Umoja wa Afrika, Morocco imekuwa ikishiriki shughuli mbalimbali za kimataifa,” alisema.
Hata hivyo, Dk Mahiga alisisitiza kwamba msimamo wa Tanzania katika suala la Sahara Magharibi ni kuitaka Morocco kuiacha huru nchi hiyo kwa sababu zama za ukoloni zilishapita.

No comments: