WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO, NAPE NNAUYE.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema kuwa Yanga haikufuata taratibu katika mchakato wake wa kubadili umiliki kwani hata Mkutano Mkuu wa wanachama uliendeshwa kienyeji.
Mbali na hilo, Nape pia alisema kuwa kabla ya kuhitimisha mkutano huo wa wanachama, uongozi wa Yanga ulitakiwa kutoa notisi ya siku 60 kwa wanachama wake kama Katiba yao inavyoagiza.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma katika kipindi cha radio moja, Nape alisema kuwa Serikali inajua kuwa Manji hafanyi kazi na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Alisema pamoja na kupitwa na wakati kwa sera ya michezo, lakini wadau wamekuwa wakisuasua kutoa mapendekezo ya marekebisho yake ili iweze kuendana na wakati.
“Mkutano ulioitishwa kwanza hakufuata taratibu, walitakiwa kutoa notisi ya siku 60 kwa wanachama wake, lakini hawakufanya hivyo, Serikali tunajua Manji hafanyi kazi na wajumbe wake wa Kamati ya Utendaji,”alisema.
Alisema kuwa sera ya michezo ina mapungufu yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuondoa manung’uniko kwa washika dau, ambao ni klabu za michezo na wanamichezo ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakilalamikia sera ya michezo kupitwa na wakati.
Wadau hao hususani wa soka wamekuwa wakilitupia lawama Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuwa ni mzigo kwani imekuwa ikipata mgao kwa kila mchezo wa ligi wa asilimia tano ya mapato, huku likiwa halitoi msaada kwa timu za taifa zaidi ya kukabidhi bendera pindi zinapoenda kwenye michuano ya kimataifa.
Hatahivyo, akizungumzia hilo, Nape alisema, “Mapungufu kwenye baraza yapo lakini hayaondoi umuhimu wa baraza kuwepo kwa sasa kwa vile ndio wanaosajili na kusimamia masuala yote ya michezo, kuna mambo mengi mazuri yanayofanywa na baraza na si kweli kuwa halifai kwa kile kitu.” “BMT imekuwa ikifanya mambo mazuri, inawezekana mtu ambaye hajahitaji huduma ya baraza hawezi kujua umuhimu wake, dunia inabadilika sioni shida kufanya mabadiliko lakini sio kulitupia mawe baraza,”alisema.
Kauli ya Nape imekuwa ikiwa ni siku chache baada ya BMT kuzuia klabu za Simba na Yanga kuendelea na mchakato wake wa mabadiliko ya umiliki hadi pale zitakapobadili katiba zake.
Kwa upande wa katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema sera ya baraza ya mwaka 71 haliendani kwa matakwa ya sasa kwa yanayoendelea ndani ya klabu za michezo.
“Soka letu la kulipwa, ngumi za kulipwa, mpira wa miguu Fifa imetoa maelekezo na katiba za mfano kwa wanachama wake na haitambui baraza kama chombo cha maamuzi ya juu. Licha ya Fifa kuitambua serikali lakini haipi kipaumbele kwenye maamuzi baraza likae chini liangalie nafasi yake kama litaendelea na majukmu yale yale au yabadilishwe,”alisema Osiah.
Hata hivyo, aliwataka watendaji wa Baraza kukaa chini na kujitafakari iwapo nguvu wanayotumia kwa wakati huu bado wanastahili kwani kuzuia mchakato wa mabadiliko kwenye klabu za Simba na Yanga si sahihi.
Wakati Osiah akisema hayo, Mwenyekiti wa zamani wa Simba na ambaye ia amewahi kuwa katibu mkuu wa FAT (sasa TFF), Ismail Aden Rage alisema “BMT ipo sahihi na ina umuhimu mkubwa na kuzitaka klabu za michezo hususani Simba na Yanga kuheshimu maamuzi ya baraza hilo.
“Kusipokuwa na chombo cha juu kama BMT kusimamia michezo itakuwa vurugu mechi kwenye nchi yetu na inaweza kutugawa, mfano mtu anaweza kuanzisha timu yake ya Wanyamwezi Football klabu akasema wanaocheza ni Wanyamwezi tu, hiyo ni hatari lakini baraza halina udini hivyo bado lina umuhimu mkubwa,”alisema.
No comments:
Post a Comment