Thursday, November 10, 2016

ALLY CHOKI KUADHIMISHA MIAKA 30 YA KUIMBA.

Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk Jim Yonazi (kulia) akisalimiana na mwanamuziki wa dansi nchini, Ally Choki wakati alipotembelea ofisi za kampuni hiyo inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na Spotileo jana, kuzungumzia tamasha lake la miaka 30 tangu aanze muziki litakalofanyika Novemba 26 mwaka huu. Wengine kutoka kushoto ni Meneja wa mwanamuziki huyo, Martin Sospeter, Mhariri wa Spotileo, Amir Mhando na msemaji wa mwanamuziki huyo, Juma Kasesa. (Picha na Abdallah Msuya).
Nyota mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Ally Choki ‘Mzee wa Farasi’ amesema anatarajia kufanya tamasha kubwa la muziki kuadhimisha miaka 30 tangu kuanza kwake kuimba mwaka 1986.
Onesho hilo litakwenda sambamba na uzinduzi wa wimbo wake mpya unaofahamika kama Natamani na uzinduzi wa kitabu kinachoelezea historia ya maisha yake ya muziki.
Choki alisema tamasha hilo litafanyika Novemba 26, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mango Garden na kushirikisha wasanii kadhaa wa zamani na sasa.
“Nimeamua kufanya ziara kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuelezea kuhusu maadhimisho ya miaka 30 ya muziki wangu, nawahimiza mashabiki wa muziki wa dansi kuja kwa wingi tusherehekee pamoja tukikumbushana burudani za zamani na za wakati huu,”alisema.
Choki alisema ataburudisha kwa nyimbo kumi, ikiwa ni mchanganyiko wa zamani na sasa ambazo zitakuwa ni kama zawadi kwa mashabiki watakaojitokeza siku hiyo.
Msanii huyo licha ya changamoto kadhaa alizopitia katika safari yake ya muziki, alisema anajivunia kupata mafanikio mengi na zaidi akisisitiza umuhimu wa watu kushiriki naye siku hiyo na kujifunza mambo mengi aliyoyaandaa kupitia kitabu chake.
Pia, amewahi kufanya kazi na bendi kadhaa za muziki nchini ikiwemo Kibaha Sound, Lola Afrika, Bantu Group, Twanga Pepeta na kuanzisha bendi yake ya Extra Bongo kabla ya kurudi tena Twanga. Nyimbo alizowahi kuimba ni Baba Jeni, Gubu la Wifi, Chuki Binafsi, Jirani na nyingine kadhaa.

No comments: