Thursday, November 10, 2016

SABABU ZA CLINTON KUSHINDWA HIZI HAPA.

HILLARY CLINTON.
Kwa nini si Hilary Clinton? Ndilo swali ambalo linaulizwa kila kona baada ya mgombea huyo wa chama cha Democtratic kuangushwa na Donald Trump wa Republican katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani.
Si rahisi kuamini Clinton kushindwa na mgombea ambaye alikuwa akihubiri sera za kibaguzi na kujenga hofu kwa baadhi ya makundi ya Wamarekani.
Wamarekani wenye asili ya Afrika na Wamexico walionekana kuwa wanamuunga mkono mke huyo wa Rais wa 42 wa Taifa hilo kubwa ulimwenguni.
Kura zao zilionekana kuwa zingeongeza idadi katika kura za raia wengine wa Marekani waliokuwa wanamuunga mkono mgombea huyo wa chama tawala kwa sasa. Lakini baada ya Trump kupata ushindi, maelezo ya kuhalalisha matokeo hayo yanayoshangaza yanaweza kueleweka.
Kwa kawaida, si rahisi kwa chama kilicho madarakani kushinda tena uchaguzi baada ya miaka minane ya vipindi viwili vya urais ukiondoa wakati George H.W. Bush alipoongoza kwa vipindi viwili na kupokelewa na Ronald Reagan, kitu ambacho ni cha kipekee.
Pamoja na utamaduni huo wa kupokezana madaraka baada ya miaka minne, kuna sababu kuu tano zinazoweza kueleza kwa nini Trump, bilionea maarufu Marekani na mtangazaji wa kipindi cha Apprentice, amefanikiwa kumuangusha Clinton aliyeonekana kuelekea kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza taifa hilo.
Kushindwa kuunganisha makundi
Moja ya sababu kuu ya kuanguka kwa waziri huyo wa mambo ya nje ni kushindwa kuendeleza nguvu ya rais wa sasa, Barack Obama ya kuunganisha makundi ya wananchi wa Marekani.
Wamarekani wenye asili ya Afrika, ya Amerika Kusini na wapiga kura vijana hawakujitokeza kwa wingi kupiga kura kuweza kumuingiza Ikulu Clinton.
Kabla ya matokeo kutangazwa, alikuwa na uhakika wa ushindi. Lakini mwishoni alijikuta akianguka kwenye majimbo yaliyoonekana yako nyuma yake, kama Wisconsin. Aliachwa kwenye majimbo mengine kama Pennsylvania na Michigan.
Wakati alikusanya kura nyingi kutoka kwenye makundi yenye watu wengi ambayo kampeni zake ziliyalenga, hakuweza kufikia idadi ambayo Obama alipata, hata miongoni mwa wanawake.
Idadi kubwa kidogo ya Wamarekani weusi na Walatino walimpa kura nyingi Trump kuliko walivyompigia Mitt Romney kwenye uchaguzi wa mwaka 2012, licha ya kauli zake kali kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika, Wamexico na wahamiaji wasio na nyaraka.
Obama, ambaye alishinda urais kutokana na msaada wa Wamarekani wenye asili ya Afrika na jamii za Kilatino, mara kadhaa aliomba wapiga kura weusi kumuunga mkono Clinton.
Lakini, Trump akatumia ujanja kushawishi Wamarekani weusi kwa kuzungumzia maisha yao halisi, akisema wanaishi maisha ya kimaskini, hawana kazi na wanauawa kila wanapotembea mitaani.
“Mtapoteza nini?” alisema katika moja ya hotuba zake.
Trump alisema maneno hayo kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni.
“Tutajenga upya makazi ya watu wa chini kwa sababu jamii za Wamarekani wenye asili ya Afrika wako kwenye hali mbaya sana kuliko walivyowahi kuwa,” alisema Trump katika moja ya mikutano yake iliyohudhuriwa na Wamarekani weupe tu.
“Angalia kwenye maeneo yao, utaona hakuna elimu, ajira na ukitembea mitaani unauawa kwa risasi. Wako kwenye hali mbaya – namaanisha, kutoka moyoni kabisa, nchi kama Afghanistan ni salama zaidi kuliko maeneo yao ya sasa.”
Clinton pia hakuwa maarufu miongoni mwa watu weupe kama alivyokuwa kwa Obama. Alipata asilimia 37 ya kura za Wamarekani weupe kulinganisha na asilimia 39 alizopata Obama. Cha ajabu ni kwamba hata Trump alipata asilimia chache kulinganisha na Romney (asilimia 58 kwa 59).
Idadi ya wapiga kura weupe ni asilimia 70, ikiwa imeshuka kutoka asilimia 72 miaka minne iliyopita.
Hata wapiga kura wenye asili ya Asia, ambao ni asilimia 4 tu, hawakumuunga mkono Clinton kama ilivyokuwa kwa Obama.
Wapigakura vijana pia hawakumuunga mkono Clinton na walifanya hivyo kwenye kura za maoni ndani ya Democratic walipompa kura nyingi mpinzani wake, Bernie Sanders na pia walipompendelea zaidi Obama miaka minne iliyopita.
Uchumi
Pia kitendo cha Trump kuwashawishi Wamarekani kuwa sera mbovu za utawala wa sasa na mipango mibovu ya biashara ndiyo iliyoharibu uchumi wa Marekani. Obama alisaidia kuunusuru uchumi wa Marekani kutoka katika janga la kuporomoka kutokana na tatizo la fedha.
Kwa bahati mbaya, kwa upande wa Clinton, Wamarekani wengi hawakuliona hilo. Mishahara isiyopanda na kukua kwa tofauti katika jamii, ni mambo ambayo wengi waliona yanawaathiri. Trump alifanikiwa kuwashawishi kuwa hiyo ilitokana na mikataba mibovu ya biashara na uendeshaji mbovu wa uchumi.
Licha ya mpinzani wake kwenye kura za maoni, Sanders kumbana katika suala hilo, Clinton hakuonekana kuwa na jibu la kutosheleza. Sura yake ya kinyonga katika masuala ya biashara ilionekana na baadaye ikathibitisha na barua pepe zilizovujishwa.
Licha ya tabia ya Trump ya kutoa kauli tata na kushambulia baadhi ya makundi kwenye jamii, Clinton alionekana kushindwa kushawishi wapigakura kuhusu uchumi.

No comments: