Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imesema kabla ya mauti kumfika mtoto Happiness Malley aliyewekewa kifaa cha moyo ‘pace maker’ aliugua kifua.
Msemaji wa JKCI, Maulid Kikondo alisema baada ya kupokea taarifa za kifo hicho walichunguza kupitia historia ya ugonjwa wake na kugundua kuwa chanzo cha kifo chake siyo mashine aliyowekewa.
Happiness alifariki Novemba 6 na alizikwa juzi Mbulu mkoani Manyara.
Elitruda Malley ambaye ni mama yake Happiness, alisema kabla ya umauti kumfika, mwanaye aliugua ugonjwa wa kifua kwa zaidi ya wiki moja.
“Baada ya kufanya uchunguzi wetu kutokana na historia yake ya awali, tukagundua kwa vyovyote vile pacemaker ingefeli angerudi katika hali yake ya awali,” alisema Kikondo.
Kikondo alifafanua kuwa pacemaker hiyo ilikuwa inamsaidia kufanya presha yake ikae vizuri na kwamba, iwapo ingefeli na angerudi katika hali yake ya kawaida na asingekufa.
“Inavyoonekana alipata maambukizi, maana wanasema alikuwa anakohoa sana inavyoonekana itakuwa nimonia. JKCI tutatoa maelezo mengine zaidi kuhusu kifo cha Happiness wiki ijayo,” alisema Kikondo.
Malley alisema kabla ya umauti kumfika mwanaye, Jumapili alikuwa mzima na walikwenda kanisani kutoa sadaka ya shukrani kwa mambo aliyowatendea na wakarudi nyumbani salama. “Jumatatu tuliamka salama lakini ghafla hali yake ilibadilika, akaanza kulalamika anajisikia vibaya, tuliamua kumpeleka hospitalini lakini kabla hatujafika Selian alikufa njiani,” alisema.
Mtoto huyo aliyezaliwa akiwa na udhaifu katika misukumo ya mapigo ya moyo, alifanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa hicho Julai 16. Mkurugenzi wa JKIC, Dk Peter Kisenge alisema operesheni hiyo ilifanyika takriban saa moja kwa mafanikio makubwa.
Operesheni hiyo ilishirikisha timu ya madaktari kumi wakiwamo mabingwa kutoka Virginia, Marekani.
No comments:
Post a Comment