MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, GEORGE MASAJU. |
Serikali imesema si kweli kuwa posho kwa watumishi wa taasisi za umma zimefutwa, bali marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma yamelenga kuipunguzia serikali gharama na tayari hatua zimechukuliwa ambapo kuanzia Julai mwaka huu, hakuna mkuu wa taasisi anayelipwa zaidi ya Sh milioni 15.
Aidha, imesema hakuna Sheria ya Utumishi wa Umma wala yoyote iliyovunjwa na Rais John Magufuli, alipofanya uteuzi wa wakurugenzi watendaji kwa kuwa Katiba ya nchi, inamruhusu kufanya hivyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakifafanua hoja za serikali wakati wa majadiliano ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali Namba 3 wa mwaka 2016, mawaziri wa wizara mbalimbali walisema Rais anaongoza nchi kwa misingi ya sheria.
Mawaziri hao walikuwa wakijibu hoja za wabunge, ikiwemo hoja ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu kuhusu muswada huo baada ya kueleza kuwa Rais amevunja sheria za utumishi wa umma, za uchaguzi kuteua baadhi ya makada wa CCM kuwa wakurugenzi watendaji, akijua kuwa watahusika kusimamia uchaguzi na hawatatenda haki kwa vyama vingine.
Akieleza kuhusu hoja hiyo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, alisema “Katika katika Ibara ya 36, inampa Rais mamlaka ya kufuta, kuanzisha na kuteua. Hakuvunja Katiba hata kidogo, amechagua watu watakaomsaidia kufikia malengo na ahadi alizotoa.”
Nape alitaka kauli hizo zipuuzwe, kwani zina lengo la kupoteza ajenda na kuwataka Watanzania kumuamini Rais katika kuwafikisha katika Tanzania mpya kiuchumi.
Akijibu hoja hiyo, Nape alisema, “Ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kurejesha nidhamu ya utumishi wa umma. Watanzania walituamini katika hilo na tunalitekeleza, wapinzani wanataka kuzuia tusitekeleze ajenda yetu”.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema nia ya serikali ni kuwianisha mishahara na posho ni njema kupunguza gharama na kuanzia Julai hakuna mkuu wa taasisi anayelipwa zaidi ya Sh milioni 15.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju katika majumuisho alisema kulikuwa na malalamiko makubwa kuhusu tofauti ya mishahara kati ya mtu wa chini na wa juu, hivyo shera hiyo imelenga kuweka usawa bila upendeleo.
No comments:
Post a Comment