Monday, September 19, 2016

TANZIA: NGULI WA MUZIKI AFRIKA KUSINI MANDOZA AFARIKI DUNIA.

Mandoza

Nguli wa muziki nchini Afrika kusini Mduduzi Tshabalala maarufu kama Mandoza amefariki baada ya kuugua saratani kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Amefariki dunia akiwa na miaka 38.

Mandoza alisifika kwa album kadhaa za mziki aina ya kwaito, aina ya mziki wa Afrika kusini ambao hukaribiana sana na Hip hop.

Nyimbo zake nyingi zilivuma zikiwemo nyimbo kutoka albamu yake ya kwanza Nkalkatha. Familia ya Mandoza imesema kuwa mwanamziki huyo aligundulika kuwa ana saratani baada ya kuanza kuumwa na kichwa sana pamoja na kutatizwa na macho mwaka mmoja uliopita.


RADI YAUA WATU NA WENGINE KUJERUHIWA SHINYANGA.

Kamanda Mkuu wa polisi mkoani Shinyanga Muliro Jumanne.

Watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa wamejikinga na mvua chini ya mti kando ya malambo ya kunyweshea mifugo katika kijiji cha Ntundu kata ya Busangi katika halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne alisema ajali hiyo ilitokea juzi 8:30 mchana katika kijiji hicho wakati mvua ilipokuwa ikinyesha, ndipo watu hao wakaamua kujikinga kwenye mti na radi ikapiga na kusababisha vifo vyao.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Fikiri Paschal (35) na Maneno Luzalia (16), wakati waliojeruhiwa na kupata mshituko baada ya radi kupiga ni watano ambao ni Mhoja Pasiani (32), Abel Feleshi (12), Nhungwa Jeremiah (22), Juma Mussa (16) na Paschal Mabula (11) ambaye ni mwanafunzi wa Ntundu.

Aliwataka wananchi kutokaa karibu na miti hasa kipindi hiki cha mvua za masika zinapokaribia kunyesha kwa wingi ili kuepuka tukio kama hilo ambalo limepoteza maisha ya watu, huku akifafanua kuwa katika mfumo wa umeme pia kuna madhara.


WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ASISITIZA KUWA HALI YA UCHUMI KWA SASA NI SHWARI.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Serikali imesema hali ya uchumi kwa sasa ni shwari kabisa na inaendelea kuimarika, si mbaya kama inavyodhaniwa na kupotoshwa na baadhi ya watu.

Aidha imesema imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi endelevu, usimamizi thabiti wa raslimali za umma na ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya mpango wa pili wa maendeleo ya miaka mitano.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu alipokuwa akielezea mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi nchini wakati akihairisha vikao vya bunge vya mkutano wa nne wa bunge la 11 lililoketi kwa wiki mbili kuanzia Septemba 6.

Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa uchumi, hususani mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa taifa, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wabunge na watanzania kwa ujumla kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika.

Aliongeza kuwa tathimini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha inaonesha kuwa benki nchini zipo salama, zina mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha.


Friday, September 16, 2016

HILLARY CLINTON AENDELEA NA KAMPENI BAADA YA KUUGUA.

Mgombea kupitia chama cha Democratic, Hillary Clinton.

Mgombea Urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani, Hillary Clinton amerejea katika kampeni baada ya kuugua homa ya mapafu.

Akiongea na mwandishi wa habari akiwa kwenye ndege kuelekea Greensboro North Carolina, Clinton alisema anajisikia vizuri baada ya mapumziko ya siku tatu.

Mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump ametoa barua kutoka kwa daktari wake kuonesha kuwa ana afya njema.

Barua hiyo inaonesha anatumia dawa ili kupunguza unene na kiwango kilichopitiliza cha uzito, lakini hatumii kilevi wala kuvuta sigara.

Uchaguzi wa Marekani utafanyika mwezi Novemba ambapo kampeni zake zimekuwa na vuta nikuvute kutoka vyama vikubwa viwili vya Democratic na Republican.


MANJI KUKODISHWA YANGA KWA MIAKA 10 KUANZIA OKTOBA.

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji anatarajiwa kukabidhiwa timu hiyo baada ya mchezo wao wa ligi kuu na Simba, Oktoba mosi mwaka huu.

Habari zilizopatikana jana zinasema, bodi ya wadhamini wa Yanga chini ya Fatuma Karume na Francis Kifukwe imeridhia kumkodisha rasmi Manji timu hiyo kwa miaka 10 kama alivyoomba kupitia mkutano wa dharura wa wananchi wa klabu hiyo uliofanyika Juni 11 mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es salaam.

Manji aliomba apewe klabu hiyo kwa miaka 10 ambapo katika kipindi hiko atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama, ambapo pia katika ukodishwaji huo timu ya soka na nembo ya klabu zote zitakuwa chini ya kampuni zake.

"Mkinikodisha ndani ya miaka mitatu nitahakikisha naingiza faida na asilimia 25 ya faida itaenda kwa wanachama wa klabu, ikiwa ni hasara nitabeba mimi na baada ya miaka kumi nitawarudishia klabu yenu, muanze kununua hisa" alisema Manji.


WABUNGE WA CUF HAWAMTAMBUI LIPUMBA.

Wabunge wote wa chama cha wananchi (CUF)  wametangaza rasmi kutomtambua aliyekuwa  mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Wamemtaka msajiri wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutomkumbatia mwanasiasa huyo aliyebobea katika uchumi, akielezwa kwa sasa hana sifa za kuwa mwenyekiti, labda aanze upya mchakato.

Wameeleza msimamo huo jana mjini Dodoma na Mbunge wa viti maalum, Riziki Mngwali ambaye pia ni kiongozi wa wabunge wa CUF katika mkutano baina ya waandishi wa habari za bunge na wabunge wa CUF isipokuwa mbunge wa jimbo la Kaliua, Magreth Sakaya aliyesimamishwa uanachama.

Mngwali alisema Lipumba amekuwa akikiyumbisha chama na hivi karibuni kudai amekaririwa akisema anasubiri barua ya msajili wa vyama vya siasa ya kuthibitishiwa kuendelea na uenyekiti wake.

"Wakati anajiuzuru uenyekiti Agosti 5 mwaka jana alitangazia umma na kudai anakwenda Rwanda kwa kazi aliyodai ya utafiti ili asaidie serikali, lakini inashangaza sasa anataka kujirejeshea uenyekiti, hilo hatukubali kwa kuwa chama kina taratibu zake" alisema.


Thursday, September 15, 2016

TRUMP AKATISHWA KUTOA HOTUBA NA MCHUNGAJI BAADA YA KUANZA KUMKASHIFU MGOMBEA MWENZAKE CLINTON.

Mchungaji wa kanisa moja la watu weusi katika jimbo la Michigan, Marekani amemkatisha Donald Trump akihutubia alipoanza kumshutumu mpinzani wake Hillary Clinton.

Mchungaji Faith Green Timmons alimkatisha Trump alipomshutumu mgombea huyo wa chama cha Democratic kuhusu mikataba ya kibiashara.

"Trump nilikualika hapa uje utushukuru kwa juhudi ambazo tumefanya Flint, si kutoa hotuba ya kisiasa" alisema mchungaji huyo wa kanisa la Bethel United Methodist.

Trump aliendelea na kuzungumza kwa kifupi kuhusu kutatua tatizo la maji safi Flint, lakini baadhi ya watu kwenye umati wakaanza kumzomea.

Mwanamke mmoja alisema kwa sauti kwamba mfanyabiashara huyo tajiri alitumia njia za kibaguzi katika kampeni yake.

Mfanyabiashara huyo alimjibu "haiwezekani umekosea, nisingeweza kufanya hivyo".

Mchungaji huyo aliingia tena na kuwashutumu waliokuwa wanamzomea Trump na kusema "yeye ni mgeni katika kanisa langu na inabidi mumuheshimu".

Trump mwishowe alilazimika kukatiza ghafla hotuba yake ambayo ilidumu kwa dakika sita hivi.


MWANAMKE AKAMATWA KWA KUIBA MTOTO MWENYE SIKU 10.

Polisi mkoani Morogoro inamshikilia Anna Luambano (33) ambaye ni mkazi wa Kipawa jijini Dar es salaam kwa tuhuma za wizi wa mtoto Angel Meck mwenye umri wa siku 10 baada ya kumlaghai mama wa mtoto huyo Maimuna Mohammed mkazi wa Chamwino katika manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa polisi wa mkoa Ulrich Matei amesema wizi huo ulitokea Septemba 13, saa tano asubuhi katika mtaa wa Kilimahewa manispaa ya Morogoro.

Akielezea mazingira ya wizi huo, Kamanda Matei alisema mtuhumiwa alimdanganya mama wa mtoto huyo wakiwa njiani kutoka kituo cha Afya Mafiga, akimwomba ampe mtoto wake akamwoneshe mume wake kuwa huyo ni mtoto wa mdogo wake, ambaye amejifungua ili awape fedha za hongera kisha wagawane.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kupewa mtoto alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mama mtoto baada ya kugundua kuwa ameibiwa alienda kutoa taarifa kituo cha polisi. Ndipo polisi walipoanza kufanya msako kwenye mabasi yote ya abiria yanayosafiri maeneo mbalimbali na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa katika basi la Upendo eneo la Mdaula mkoani Pwani akienda mkoani Dar es salaam.

Mtuhumiwa alikiri na kusema hakuwa na nia mbaya bali alitaka kwenda kumlea huyo mtoto.


LOWASA AMKOSOA RAIS MAGUFULI.

Lowassa

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Edward Lowasa amemkosoa mpinzani wake rais Magufuli kwa kile alichokitaja ni udikteta nchini humo.

Akizungumza na mwandishi wa BBC nchini Kenya, alisema kuwa alitarajia kwamba Magufuli angeondoa urasimu serikalini lakini kuna mambo mengi hayajakwenda sawa, japokuwa alikataa kutoa mifano alipotakiwa kufanya hivyo.

Lowasa alikuwa katika chama tawala alipokuwa Waziri Mkuu, lakini mwaka uliopita alijiunga na upinzani wa CHADEMA ambapo alishindwa na Rais Magufuli wakati wa uchaguzi.

Magufuli alipewa jina tinga (Bulldozer) anajulikana kufanya maamuzi yanayopendwa tangu achukue madaraka mwaka uliopita, kama vile kufutilia mbali sherehe za Uhuru ili kuhifadhi pesa.


Wednesday, September 14, 2016

VIDEO YA WIMBO WA RARUA WA MALAIKA WAZUA UTATA.

Malaika

Wiki iliyopita video ya wimbo wa Rarua wa mwanamziki Malaika ulitoka huku Hanscana akiwa ni director wa video hiyo.

Taharuki imetokea pale ambapo aliyekuwa mpenzi wa Malaika, kijana Eddy ambaye siku za nyuma alikataza nyimbo hiyo kutoka, kutokana na kulipa gharama zote lakini Malaika akamzingua kwa kumshitaki polisi kuwa alimtishia maisha.

Leo katika kipindi cha XXL kinachorushwa na Clouds Fm, Eddy alisikika kwenye Uheard akisema wimbo huo haukutakiwa kutoka na walikubaliana na Hanscana wasitoe nyimbo hiyo mpaka watakapokubaliana.

Lakini wimbo umetolewa na Eddy katishia kuufunga kwani umetolewa bila makubaliano na yeye ndiye aliyegharamia wimbo mzima.


MHANDISI ASAFIRI KWA KUTUMIA BAJAJI ISIYOTUMIA MAFUTA KUTOKA INDIA MPAKA UINGEREZA.

Mhandisi kutoka India ambaye amekuwa akiendesha bajaji ya kutumia makawi ya jua amewasili Uingereza baada ya safari iliyodumu miezi saba.

6,200 mile (9,978km) umbali wa safari.

Naveen Rabelli ambaye ni mzaliwa wa Australia aliendesha bajaji yake kutoka kwenye feri dover, Uingereza akiwa amechelewa kwa siku tano.

Alitarajia kufika mapema lakini akakwama kwa mda Paris baada ya pasipoti na kipochi chake kupotea.

Lengo lake la kufanya ziara hiyo ilikuwa kuhamasisha watu kutumia magari yanayotumia kawi mbadala kama vile sola na umeme.

Anapanga kuhitimisha safari yake katika kasri la Buckingham, London.

Alianza safari yake Bangalore nchini India kisha akaendea Iran, alipitia Uturuki, Bulgaria, Serbia, Austria, Uswizi, Ujerumani na Ufaransa.


WABUNGE WA UINGEREZA WATAKA BANGI KUHALALISHWA.

Mmea wa bangi.

Kundi moja la wabunge nchini Uingereza limetoa wito wa kuhalalishwa kwa matumizi ya bangi kwa sababu za matibabu nchini humo.

Kundi hilo linalojumuisha wabunge mbalimbali kutoka vyama vya siasa na ambalo limekuwa likitetea mageuzi kuhusu matumizi ya dawa, limesema kuna ushahidi bayana kwamba matumizi ya bangi huwa na manufaa katika kutibu baadhi ya magonjwa ya kiafya, yakiwemo maumivu makali na kutatizwa na wasiwasi.

Wabunge hao wanasema tayari maelfu ya watu huvunja sheria kwa sasa na kutumia bangi kama dawa.

Lakini wizara ya mambo ya ndani nchini humo imesema kufikia sasa hakuna mipango ya kuhalalisha matumizi ya dawa hiyo hatari.

Mmea wa bangi huwa na karibu na kemikali 60.

Wabunge hao wanataka serikali iondoe bangi kutoka kwa kitengo nambari moja hadi kitengo  nambari nne.

Kitengo hicho kina dawa nyingine zikiwemo homoni, vitamin na dawa za kupunguza maumivu.

Hii itawawezesha madaktari kumpendekezea mgonjwa kutumia bangi kama dawa.

Taasisi ya Afya ya Uingereza imetahadharisha kwamba bangi huwa na madhara makubwa kwa mwili, ikiwemo kutatiza uwezo wa mtu kuendesha gari na kudhuru mapafu na afya ya kiakili, kuathiri uwezo wa mtu kuzaa na kuathiri pia watoto ambao hawajazaliwa.

Bangi pia huwa na kiwango cha utegemezi cha 9%, ingawa si cha juu sana kulinganisha na tumbaku 32% na pombe 15%.

Lakini wabunge hao wanasema wametathimini ushahidi kutoka kwa wagonjwa 623 pamoja na kuzungumza na wataalamu kutoka nchi nyingi duniani na wamegundua bangi inaweza kufaa sana kama dawa.

Nchi kumi na moja zimehalalisha kutumia bangi kwa sababu za kiafya.

Majimbo 24 nchini Marekani na pia nchini Canada na Israel wamehalalisha matumizi ya bangi.


MWANARIADHA MLEMAVU KUTOKA NCHINI KENYA AMESHINDA DHAHABU KATIKA MASHINDANO YA PARALIMPIKI.

Mwanariadha mlemavu kutoka nchini Kenya Samwel Mushai Kimani ameshindia Kenya dhahabu nyingine baada ya kuibuka mshindi wa mbio za wanaume mita 1,500 kitengo T11 Paralimpiki.

Kimani aliandikisha muda wa 4:03,25 muda bora zaidi msimu huu.

Mbrazil Odair Santos alimaliza wa pili.

Mbio hizo hata hivyo hazikuwa za kasi kama za kitengo T13 ambapo wanariadha wanne waliomaliza wa kwanza waliandikisha muda bora kushinda wa mshindi wa mbio za Olimpiki mita 1,500.

Kimani alikuwa ameishindia Kenya dhahabu ya kwanza katika michezo ya Olimpiki ya walemavu wa Rio 2016 kwa ushindi katika mbio za mita 5,000 kitengo T11.

Kenya ilishinda dhahabu mbili Paralimpiki za London na kubeba medali sita kwa ujumla.


FEDHA ZACHANGWA ZA KUWASAIDIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO BUKOBA.

Wakati vifo vya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera vikiongezeka na kufikia 17, uongozi wa mkoa huo umesema zinahitaji zaidi ya bilioni 2.3 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya waathirika, tayari serikali jana imehamasisha na kupatikana zaidi ya bilioni 1.4.

Kati ya fedha hizo zilizopatikana Sh.milioni 700 zilikuwa ahadi, fedha taslimu Sh.milioni 646, Dola za marekani 10,000, Euro 10,000 na mifuko 2,800 ya theruji.

Mahitaji yanayohitajika ya haraka ni
- Dawa, tiba na vifaa tiba.
- Vifaa vya ujenzi, mabati 90,000 yenye thamani ya bilioni 1.7.
- Saruji mifuko 9,000 yenye thamani ya sh.milioni 162, mbao na misumari.

Kampuni za mafuta ya Oilcom, GBP na Moil zimejitolea kujenga shule mbili za sekondari zilizoathirika na tetemeko hilo.

-Reginald Mengi alichangia ml.110.
-Mohammed Dewji alichangia ml.100.
-Chama cha wauzaji mafuta kwa rejareja walichangia ml.250.


WAANDAAJI WA TUZO ZA EATV KUANZA KUTOA FOMU KWA WASANII.

Zoezi la wasanii kuchukua fomu za kushiriki kwenye tuzo za mwaka huu za EATV limefunguliwa jumanne hii.

Akiongea kupitia kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Televisheni, Mkuu wa masoko wa EATV, Roy Mbowe alisema mwisho wa kuchukua fomu na kuzirudisha ni Oktoba 22 saa 11 jioni.

Amesema fomu zinaweza kujazwa na msanii mwenyewe au meneja wake, lakini pia lazima kuwepo na mashahidi watakaojaza pia. Wasanii watatakiwa kuzirudisha fomu hizo pamoja na kazi zao.

Fomu hizo zinapatikana kwenye tovuti ya http://www.eatv.TV/awards.

Tuzo hizo zitakuwa na vipengele 10 zitakazohusisha muziki, filamu na tuzo moja ya heshima.

Vipengele hivyo ni;
1. Mwanamuziki bora wa kiume.
2. Mwanamuziki bora wa kike.
3. Mwanamuziki bora chipukizi.
4. Kundi bora la muziki.
5. Video bora ya miziki.
6. Wimbo bora wa mwaka.
7. Muigizaji bora wa kiume.
8. Muigizaji bora wa kike.
9. Filamu bora ya mwaka.
10. Tuzo ya heshima itakayotolewa kwa mtu au kampuni iliyochangia kwa kiasi kikubwa katika kazi ya muziki.


WALIMU WACHARAZWA NA WANAFUNZI.

Wanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Usevya wilayani Mlele mkoa wa Katavi wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwachapa viboko walimu wao wawili miongoni mwao akiwa makamu mkuu wa shule hiyo, Makonda Ng'oka "Membele" (34) ambaye ameng'olewa meno matano kwa kipigo hicho.

Walimu hao wamedai kuwa hawapo tayari kufundisha katika shule hiyo huku wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kuchapwa viboko na wanafunzi wao wenyewe ambapo mwalimu, Gabriel Kambona aliachwa na ngeu kichwani.

Mei mwaka huu Ng'oka alifikishwa mahakamani kwa kosa la kumlawiti mwanafunzi wake.

Ilisemekana kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makamu mkuu huyo wa shule hiyo kulifuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma kidato cha tano sasa wapo kidato cha Sita katika shule hiyo kumkataa na kutishia kuandamana kupinga vitendo vyake vya kulawiti wasichana.

Baada ya mda mwalimu Ng'oka aliachiwa huru na kurudi shule. Kurudi kwake hapo shuleni kunadaiwa kurejesha hasira za wanafunzi wa kidato cha Sita wakidai hawapo tayari kumuona mwalimu huyo na familia yake shuleni hapo.

"Sipo tayari kuendelea kufundisha katika shule hii, wanafunzi watatumaliza Mimi na familia yangu" alisema Ng'oka.


Tuesday, September 13, 2016

KIBAHA KUKUMBWA NA BOMOABOMOA NOVEMBA.

Wakazi wa Kiluvya Mailimoja hadi Tamko Kibaha waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro wametakiwa kubomoa majengo yao kabla ya bomoabomoa kuanza Novemba 24.

Bomoabomoa hiyo itawahusu wakazi ambao majengo yao yapo ndani ya mita 60 kila upande wa barabara na ambao tayari nyumba zao zimeekewa alama ya X kuwataarifu kuwa wamejenga sehemu sio sahihi.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema katika kikao cha bodi ya barabara kuwa wananchi watambue kuwa taarifa walizopewa za kubomolewa nyumba zao ni za kweli na itahusisha nyumba zote zilizo ndani ya mita 60 kila upande na sio 120 kama ilivyosemwa awali.

Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Asumta Mshama alisema "mimi bado naona tunawasumbua hawa wananchi wakati hawana tabu ya kuondoka. Wote waliowekewa X wanajua siku yoyote wanatakiwa kuondoka".


VITAMBULISHO VYA TAIFA KUBADILISHWA.

Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani ambavyo havina saini, huku ikitarajia kutoa vitambulisho vipya vyenye saini kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi kwa kuchukuliwa alama ya kibayologia ikiwemo alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki.

Aidha inatarajia kutoa vitambulisho vipya kuanzia Septemba 14 katika ofisi zote za NIDA za wilaya. Taarifa iliyotolewa jana Dar es salaam na Kaimu mkurugenzi mkuu wa NIDA Andrew Massawe alisema kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika pamoja na vipya huku taratibu za kubadilisha zikiendelea.


Monday, September 12, 2016

WAFUASI WA DINI YA KIISLAMU WASHEREHEKEA SIKUKUU YA EID EL HAJJ.

Leo ni sikukuu ya Eid El Hajj ambapo Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limewataka waislamu wote nchini kusherehekea kwa amani, huku wakiwakumbuka wenye matatizo, kuwa wepesi wa kutoa sadaka na isiwe siku ya kutenda maovu.

Katibu mkuu wa Bakwata, Shehe Suleiman Lolila alitangaza jana kuwa leo ni sikukuu ya Eid el hajj na kuongeza kuwa kitaifa sherehe hizo zitafanyika katika makao makuu ya Bakwata yaliyopo Kinondoni jijini Dar es salaam.

Alisema mgeni rasmi katika sherehe hiyo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambapo sala itaanza mapema saa moja asubuhi na Baraza la idd kuanza 2:30 hadi saa 4:00 asubuhi.

Idd El Hajj inahitimisha ibada ya hija kwa waumini mbalimbali wa dini ya kiislamu huko Makka nchini Saud Arabia, ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za dini ya kiislamu ambayo hutakiwa kutekelezwa mara moja kwa watu wenye fedha.

Angie Blog na uongozi mzima unawatakia sikukuu njema.


HILLARY CLINTON AUGUA KATIKA KUMBUKUMBU YA WAHANGA WA SHAMBULIO LA SEPTEMBA 11.

Clinton akisaidiwa kuingia kwenye gari.

Mgombea uraisi kupitia chama cha Demokratic Hillary Clinton amegundulika kuwa na ugonjwa wa homa ya mapafu baada ya kuugua katika maadhimisho ya kuwakumbuka wahanga wa shambulio la Septemba 11.

Daktari wake Lisa Bardack amesema kuwa Clinton amekutwa na ugonjwa huo toka ijumaa.

Amesema pia Clinton aliongezeka joto na kuishiwa na maji mwilini katika maadhimisho hayo.

Clinton aliondoka mapema, picha zilizowekwa mtandaoni zinamuonesha akisaidiwa na msaidizi wake huku akitaka kuanguka alipokaribia kwenye gari. Lakini kwa sasa anaendelea vizuri.


WALIOKUFA NA TETEMEKO WAZIKWA JANA.

Maafa zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi, lililotokea juzi mkoani Kagera ambapo imeripotiwa idadi ya vifo kuongezeka na kufikia 16 huku wengine 253 wakijeruhiwa na kusababisha simanzi na masikitiko kwa familia nyingi.

Pia nyumba 840 za makazi zimeanguka, nyumba 1,264 zimepata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule yameanguka.

Tukio hilo limemfanya Waziri mkuu Kassim Majaliwa kulazimika kufanya ziara ya ghafla ya kuwatembelea waathirika wa tukio hilo na kuhudhuria ibada ya mazishi iliyofanyika siku ya jana.


AKAMATWA KWA KOSA LA KUTOA MIMBA NA KUFUKIA MWILI WA MTOTO.

Jeshi la polisi mkoani Shinyanga linamshikilia msichana, Elizabeth Benjamin (20) anayedaiwa kutoa mimba ya miezi nane na kisha kufukia mwili wa mtoto. Viungo vya mwili wa mtoto huyo vilizagaa hovyo mtaani huku mbwa wakifanya kitoweo.

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa, Elias Mwita amethibitisha leo kukamatwa kwa msichana huyo Septemba 9, mwaka huu.

Alidakwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema. Polisi walimkamata nyumbani kwake mtaa wa Butengwa kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga.

Mwita amesema katika mahojiano msichana huyo alikiri kufanya kitendo hicho na kueleza kuwa katika maelezo ya awali msichana huyo alieleza kuwa yeye ni mfanyakazi wa bar iliyopo manispaa ya Shinyanga.

Alisema bado wanaendelea na mahojiano na baada ya kukamilika watamfikisha mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Wakazi wa mtaa huo Tuma Masanja na Monica Hassan walipozungumza na mwandishi wa habari walisema kuwa baada ya tukio kutokea hawakufahamu aliyehusika na unyama huo.

Lakini baada ya siku moja walishangaa kuona askari wakifika kwenye nyumba aliyokuwa anaishi mwanamke huyo, aliyefika hapo kumtembelea dada yake, ambapo alikiri kutoa mimba ya miezi sita na kufukia mwili wa mtoto nje ya nyumba.

"Sisi tulishangaa kuona msichana huyo anaongoza moja kwa moja akiwa na askari kwenye eneo ambalo anadai alimfukia mtoto, wakajidhihirisha na kumuona hali yake ilivyo kisha wakaondoka naye kwenda kituoni lakini dada yake alikuwa akikataa kuwa ndugu yake si mhusika wa tukio hilo" alisema Monica.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Derefa alisema kuwa msichana aliyetupa mtoto na viungo vyake kuzagaa ovyo mitaani amepatikana na tayari ameshikiliwa na jeshi la polisi, ambapo lilibaini kuwa alikuwa mjamzito.


Sunday, September 11, 2016

WAISLAMU WAANZA HIJA.

Takribani mahujaji wa kiislamu ml1.5 wamekusanyika nchini Saud Arabia chini ya ulinzi rasmi kabla ya kuanza rasmi hija ya kila mwaka.

Magari yamepigwa marufuku ya kukaribia msikiti mkuu, Grand Mosque ambao ni eneo takatifu zaidi kwa waislamu, huku mahujaji wakifanyiwa ukaguzi na polisi katika vituo kadhaa kwenye eneo hilo.

Zaidi ya mahujaji 2000 waliaga dunia mwaka jana wakati wa ibada ya hija wengi wao wakiwa raia wa Iran.

Iran iliilaumu Saud Arabia kwa kutoisimamia hija inavyotakiwa na imewakataza raia wake kwenda Saud Arabia kuadhimisha ibada ya hija.


TETEMEKO LA ARDHI YAIKUMBA BAADHI YA MIKOA TANZANIA.

Tetemeko la ardhi lenye uzito wa 5.7 katika vipimo vya Richter limekumba eneo la kaskazini magharibi mwa Tanzania karibu na Ziwa Victoria.

Limetokea katika mikoa mitatu Mwanza, Kagera na Mara nchini huku watu zaidi ya 10 wamefariki na 120 majeruhi na majengo kuharibika.

Tetemeko hilo lilitokea majira ya saa tisa alasiri. Nyumba zaidi ya 47 zimeathirika, barabara zimepata mipasuko na majengo kuwaangukia watu na kusababusha vifo na majeruhi.

Mitetemeko mingine midogo ilisikika katika mataifa jirani ya Kenya na Rwanda.


Friday, September 9, 2016

MREMBO MWENYE NDEVU ALIYEVUNJA REKODI DUNIANI.

Mwanamitindo mwenye ndevu za urefu wa inchi Sita ametambuliwa na Guinness World Record kuwa mwanamke wa umri mdogo zaidi  duniani kuwa na ndevu zilizokomaa.

Harnaam Kaur, 24 ambaye ni mwanamke mtetezi wa kutambuliwa na kukubalika kwa hali ya mwili wa binadamu ulivyo bila ubaguzi. Anatokea Slough, Berkshire nchini Uingereza.

Ameeleza ndevu hizo ndefu kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na watu wengi waliomkejeli kutokana na muonekano wake.

Kaur ana tatizo la homoni lifahamikalo kwa kiingereza kama Polycystic ovary syndrome, ambalo humfanya mwanamke kuwa na nywele zaidi kuliko kawaida usoni.

Machi 2016 Harnaam Kaur alikuwa mwanamke wa kwanza kushiriki maonyesho ya mitindo ya London Fashion week akiwa na ndevu.


WANAHABARI NCHINI KENYA WAANDAMANA.

Waandishi wa habari nchini Kenya wameandamana Nairobi na miji mingine kupinga kile wanachosema ni kuongezeka kwa visa vya wanahabari kutishiwa na hata kuuawa.

Maandamano yaliitishwa na chama cha waandishi wa habari ambacho kinasema wanahabari watano wamefariki katika hali ya kutatanisha katika kipindi cha mwaka mmoja.

Maandamano yamefanyika siku kadhaa baada ya mwandishi wa habari za kisiasa kufariki katika mazingira ya kutatanisha eneo la Kilifi, pwani ya Kenya.

Katika waraka wao waliotuma kwa bunge waandishi hao walilalamika kuhusu namna watakavyoshambuliwa na kupokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa wanasiasa na umma.

Wamesema baadhi ya viongozi wa kisiasa wa serikali kuu, kaunti pamoja na raia wamekuwa wakijiamulia wenyewe kuchukua sheria mkononi na kuwashambulia waandishi wa habari kwa kuwapiga na kuwatusi kwenye mitandao ya kijamii na baadhi yao kuwatishia mauaji endapo hawatotoa taarifa zinazowapendelea.

Wamesisitiza kuwa wanayo haki ya kikatiba ya kutangaza taarifa.


KAMANDA SIMON SIRRO AKANUSHA UVUMI WA KUKAMATA WANAOPUMZIKA GUEST MCHANA.

Kamanda Simon Sirro

Kamanda wa polisi kanda kuu ya Dar es salaam, Simon Sirro ametoa rai kwa wakazi wa jiji hilo na wageni wanaoingia jijini humo kutoka mikoa mbalimbali kupuuza taarifa za sauti zinazosambazwa katika mitandao ya jamii kuwa polisi wanawakamata ovyo wanaolala mchana kwenye nyumba za wageni.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Sirro leo, habari zinazosambazwa katika mitandao ya Whatsapp na Telegram pamoja na zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti kuwa polisi wanawakamata watu hao kwa madai ya uzururaji na uzembe ni uvumi.

Kamanda Sirro alisema kwa nia ovu, taarifa hizo zimedai kuwa hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Rais Magufuli la "Hapa kazi tu" jambo ambalo si la kweli.

"Ninawatoa hofu raia wema kuwa tunaendeleza operesheni kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali wakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria kwa kuendesha guest bubu" alisema.

Amesema uchunguzi umebaini kuwepo kwa nyumba za wageni zinazoendesha biashara kiholela kwa kuhifadhi wahalifu wakiwemo wanawake na wanaume wanaouza miili yao (dada na kaka poa).

Ni wajibu wa polisi kufanya ukaguzi Mara kwa Mara kwenye nyumba za wageni, hotelini, migahawani, vilabu vya vileo na kumbi za starehe zinazokesha, alisema na kuongezea kuwa watakaobainika watakamatwa.

Sirro amewataka wafanyabiashara wa nyumba za wageni kufuata taratibu za kuandikisha wageni majina yao kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanazotoka na watakapomtilia mashaka mteja yoyote watoe taarifa kwenye kituo chochote cha polisi.


KOCHA WA ZAMANI WA TIMU YA TAIFA AFARIKI.

Kocha wa zamani wa timu ya taifa (Taifa Stars) na timu kadhaa za ligi kuu katika miaka ya nyuma, Mohammed Msomali amefariki dunia ghafla jana alasiri akiwa amejipumzisha chumbani kwake.

Msomali pia aliwahi kushika nyadhifa za kuwa mwenyekiti wa makocha wa mkoa wa Morogoro kwa kipindi kirefu kabla ya kustaafu na nafasi yake ikanyakuliwa na kocha mkongwe John Simkoko.

Chama cha makocha mkoa wa Morogoro kupitia mwenyekiti wake Simkoko kilithibitisha  kupokea taarifa ya kifo cha nguli huyo ambaye pia aliwahi kuifundisha Moro United mwanzoni mwa miaka 2000.


Thursday, September 8, 2016

TAIFA STARS YAZAWADIWA MILIONI 21.5 NA GAVANA WA NIGERIA.

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limetuma salamu za shukrani kwa Gavana wa Jimbo la Akwa Ibom, Gabriel Emmanuel kwa zawadi ya dola 10,000 za kimarekani ( sawa na sh. 21.5 milioni) kwa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars).

Hiyo ni baada ya kuonesha mchezo mzuri na wapinzani dhidi ya wenyeji Super Eagles ya Nigeria uliofanyika uwanja wa kimataifa wa Godswill Akpabo mjini humo.

Taifa Stars ilicheza mechi hiyo Jumamosi Septemba 3 2016, katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON 2017).

Katika mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure Taifa stars ilifungwa bao 1-0 mara baada ya kuibana Super Eagles hivyo kumsukuma Gavana huyo kuandaa hafla ya chakula cha jioni ambako mbali ya kuizawadia stars, aliizawadia pia Super Eagles dola 35,000 za Marekani.

Taifa Stars ilitua Dar es salaam usiku wa kuamkia leo Septemba 5 ambako baadhi ya wachezaji walipelekwa katika hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya jiji la Dar es salaam, wakati wengine hususani wale wa timu ya Azam FC walichukuliwa na viongozi wao kwa ajili ya safari ya kwenda Mbeya ambako Jumatano wanatarajiwa kucheza na Tanzania Prison kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara utakaofanyika uwanja wa Sokoine mjini humo.

Wakati nyota 18 wakitua Dar es salaam, Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta aliishia Nairobi, Kenya ambako aliunganisha ndege ya kwenda Brussels, Belgium.


MFAHAMU BINADAMU MWENYE UMRI MKUBWA DUNIANI.

Mzee Mbah Ghoto

Mzee huyu kwa jina la Mbah Ghoto kutoka Indonesia anayetokea kisiwa cha Java anaamini ndiye binadamu mzee kuwahi kuishi.

Amesema ameishi muda zaidi kushinda wake zake wanne, ndugu zake 10 na watoto wake wote.

Huwa najaribu kuwa mvumilivu na kuamini kuwa kuna watu watakaonitunza.

Nimeishi mda mrefu kwa sababu nina watu wanaonipenda na kunitunza. Mimi bado navuta sigara.

Mjukuu wake Suryanto anasema kuwa kwa mujibu wa stakabathi za serikali, Mbah Ghoto ana miaka 145 alizaliwa 31 Disemba 1870.

"Tunaamini stakabathi hizi ni halali kwa mujibu wa nyaraka rasmi za serikali. Tunaamini tarehe yake ya kuzaliwa ni sahihi" anasema Afisa wa serikali Wahyu.

"Siku ya Uhuru alikuwa akialikwa kusimulia yaliyokuwa yakitokea wakati wa vita. Anaweza kusimulia kuhusu vita dhidi ya wakoloni kutoka Japan na Waholanzi" anasema afisa huyo.

Mjukuu wake anasema Mzee huyo huwa hana masharti mengi na huwa haitishi chakula maalum.

"Kitu pekee alitutaka tufanye ni kumnunulia jiwe la kaburi lake" alisema mjukuu.

Mzee huyo anasema kwa sasa anaishiwa na nguvu na hawezi kutarajia aishi muda mrefu zaidi.

Sina nguvu kama zamani, hata kutembea ni shida. Nilikuwa mkulima na nilivua samaki mtoni, sitaki kuendelea kuishi sana ndio maana nimeandaa kaburi, ili nikifariki kila kitu kiwe tayari, alisema.

Mtu ambae aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka Ufaransa aliisha miaka 122 na siku 164. Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.


VOLKSWAGEN KUANZA KUTENGENEZA MAGARI YAO KENYA.

Volkswagen

Kenya imetia saini ya makubaliano na kampuni ya Volkswagen ya Afrika kusini ili kuanza kutengeneza magari hayo katika taifa la Afrika Mashariki kulingana na taarifa ya serikali.

Volkswagen imeingia katika mkataba huo kwa kutumia kampuni ya kutengeneza magari nchini Kenya KVM mjini Thika kuunganisha sehemu za magari hayo ikianza na gari yake maarufu la Volkswagen Vivo.

Thika ni mji wa viwanda uliopo kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi na serikali ya Kenya inamiliki hisa katika kampuni hiyo.

Gari la kwanza la Volkswagen Vivo linatarajiwa kuunganishwa katika kiwanda hicho kufikia mwezi Disemba.

Kampuni hiyo ya Ujerumani ilikuwa ikifanya operesheni zake Kenya katika miaka ya 60 hadi mwaka 1977, ikiunganisha mabasi ya Volkswagen, mabasi madogo na matatu ya kombi iliokuwa maarufu sana wakati huo.


TAYLOR SWIFT AACHANA NA MPENZI WAKE TOM.

Tom Huddleston na Taylor Swift.

Taylor Swift na Tom Huddleston wameachana baada ya kuwa na uhusiano wa miezi mitatu.

Uvumi ulianza kwamba wapenzi hao ambao walipewa jina la utani HiddleSwift walikuwa pamoja baada ya kuonekana wakitaniana katika tamasha la Met Gala mnamo mwezi Mei.

Tangu wakati huo wamekuwa pamoja katika kila pembe ya dunia ikiwemo ziara ya Uingereza kuonana na familia ya Tom.

Lakini imeripotiwa kwamba wameshindwa kuendeleza penzi lao.

Hakuna tamko lolote rasmi kutoka kwa Tom wala Taylor lakini watu wanaowafahamu wapenzi hao wameongea.


BINTI ANAYEANDIKA KWA KUTUMIA ULIMI WAKONTA KAPUNDA APATA VIFAA.

Wakonta Kapunda

Unamkumbuka Wakonta Kapunda? Binti mtanzania mwandishi wa miswada ya filamu anayeandika kwa kutumia ulimi?

Wakonta alipata ajali siku ya mahafali yake ya kidato cha sita miaka minne iliyopita. Ajali hiyo ilimuacha akiwa amepooza kuanzia shingoni na kushuka chini na kumfanya kutoweza kutumia mikono yake kuandika.

Wiki kadhaa zilizopita, BBC iliporusha habari yake msamaria mwema mmoja aliguswa na kumsaidia.

Kupitia kipindi cha Televisheni Focus on Africa katika BBC World Service mwanadada Olivia Soko kutoka Afrika ya Kusini aliguswa kufanya kitu kumsaidia Wakonta.

Akiwa mkurugenzi wa kampuni ya WhirlMarket  Technologies, Olivia alijitolea kutoa msaada wa programu ya kompyuta iitwayo Nuance Dragon Naturally Speaking.

Jinsi programu hii inavyofanya kazi ni kwamba mtumiaji yeye anazungumza anachotaka kukiandika kupitia kipaza sauti chake halafu programu hiyo inaandika yenyewe katika kompyuta ya mtumiaji.

Wakonta alijaribu kuitumia jana akaifurahia, lakini bila shaka atahitaji muda zaidi ili aizoee vizuri.


WAPINZANI NCHINI ZIMBABWE WANYIMWA CHAKULA.

Tume ya haki za binadamu nchini Zimbabwe imesema kuwa watu wanaounga mkono wapinzani, walio kwenye maeneo ya ukame wamenyimwa misaada ya chakula na chama tawala cha ZANU-PF.

Mwenyekiti ya bodi maalum Elasto Mugwadi amesema kuwa kwa sasa uchunguzi umebainisha kuwa watu wanaounga mkono upande wa upinzani wanaambiwa waziwazi kuwa hawatopewa msaada wowote wa chakula na inaarifiwa kuwa watu wengi wameathirika kutokana na hali hiyo.

Taarifa ya serikali inaonyesha kuwa nusu ya wakazi wa vijijini wamekumbwa na njaa, jambo linalochochea kupingwa kwa utawala wa Rais Mugabe.

Wakati huo huo mahakama kuu nchini humo imebatilisha marufuku ya maandamano yaliyokatazwa na polisi kwenye mji mkuu wa Harare. Ambapo marufuku hiyo ilidumu kwa muda wa wiki mbili.

Wanaharakati wanne wanaopinga utawala wa Rais Mugabe ndio waliwasilisha pingamizi mahakamani kupinga uamuzi wa polisi kupiga marufuku maandamano.

Hakimu wa mahakama kuu wa nchini humo, amesema kuwa marufuku hiyo ilikuwa batili. Siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wimbi la maandamano nchini Zimbabwe.


MICHUANO YA OLIMPIKI YA WALEMAVU KUANZA LEO BRAZIL.

Michuano ya Olimpiki kwa watu walemavu inatarajiwa kuanza leo mjini Rio de Janeiro nchini Brazil. Waandaaji wa michuano hiyo wameahidi kuwepo kwa shamra shamra za kila namna katika sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo ambayo lengo lake ni kuleta changamoto kwa watu wenye mitizamo tofauti kwa walemavu na hivyo kupitia michuano hiyo dhana hiyo itatupiliwa mbali kutokana na uwezo utakaooneshwa na wachezaji wa jamii ya walemavu.

Moja ya changamoto kubwa katika michuano hiyo ya Olimpiki ni kubugikwa na mgogoro wa kifedha pamoja na mauzo ya tiketi ya ufunguzi wa michuano hiyo kwenda mwendo wa Kobe.

Michuano hiyo inatarajiwa kushirikisha wanariadha zaidi ya elfu nne kutoka mataifa mia moja na sitini ulimwenguni watakaokuwa katika gwaride la ufunguzi, ingawa miongoni mwa hao wanariadha wa kutoka nchini Urusi hawamo.

Wanamichezo wa Urusi wamepigwa marufuku kushiriki michuano hiyo kutokana na wasiwasi  wa utumizi wa dawa za kusisimua misuli ambazo zilipigwa marufuku michezoni, inaelezwa kuwa sherehe za ufunguzi wa michuano hiyo zitashuhudiwa na mamilioni ya  watu ulimwenguni kote.


MGANGA ACHOMWA MOTO BAADA YA KUMUUA MJUKUU WAKE.

Wananchi katika kijiji cha Kalundi Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa wanadaiwa kumuua kisha kumteketeza kwa moto mganga wa kienyeji, Patrick Mwandaliwa (44) wakimtuhumu kumuua mjukuu wake, Silvia Mwanakatwe mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema tukio hilo lilitokea Septemba 4, saa mbili usiku, kijijini Kalundi wilayani Nkasi mkoano humo.

Akisimulia mkasa huo kamanda Nkasi alidai usiku wa tukio Mwandaliwa alikutana na mpwa wake Maria Kapele (21) dukani kijijini humo akiwa amembeba mtoto wake wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Mwandaliwa alimuomba mpwa wake huyo mjukuu wake huyo kisha akaondoka naye mpaka nyumbani kwake, mpwa wake hakuwa na wasiwasi wowote kwakuwa aliyemchukua mwanae ni mjomba ake.

Maria alihisi ni mda mrefu umepita tangu mjomba ake amchukue mtoto wake ndipo alipomtuma mtoto wa jirani yake kwenda kumchukua, lakini alipofika kwa Mwandaliwa alikuta mlango umefungwa akarudi na kumtaarifu mama wa mtoto.

Inadaiwa kuwa mama mtoto alipofika kwa mjomba ake ampe mtoto, alikana na kusema yeye hana mtoto wake. Ndipo Mwandaliwa alipomsukuma mpwa wake na kuingia ndani na kufunga mlango.

Mwandaliwa alipanga magunia ya mahindi mlangoni akizuia mtu yoyote yule asiweze kufungua mlango, ndipo mama mtoto alipopiga mayowe kuomba msaada kwa watu.

Watu walikusanyika katika eneo hilo la tukio, kwa kuwa walikuwa wengi waliweza kuvunja mlango na kuingia ndani na kumkuta Mwandaliwa akiwa ameshika ndoo ya plastiki mkononi akiwa na mwili wa mtoto, tayari akiwa amekufa, akiwa amemtoboa shingoni kwa kitu cha ncha Kali.

Ndipo wananchi wakiwa na silaha za jadi walimvamia Mwandaliwa na kumpiga sana kisha kumchoma.

Mwili wa Mwandaliwa ulizikwa chini ya uangalizi wa askari kwa sababu wananchi waligoma kumzika.


APPLE YAZINDUA IPHONE 7.

Kampuni ya Apple imezindua simu zaidi ya iPhone Jumatano. Uzinduzi huo ulifanyika siku chache baada ya washindani wao wakubwa wa Samsung kulazimika kusitisha kuuza simu zake za Note 7 kutokana na matatizo ya betri.

Wachanganuzi wa masuala ya teknologia wanaendelea kujadili kuhusu sifa na vifaa vipya ambavyo huenda vikawepo kwenye simu hiyo mpya.

Wengi walitarajia Apple itupilie mbali suala la tundu la kuwekea headphone jack, na badala yake kuwa na tundu moja pekee.

Hili litawafanya watumiaji wa simu hizo kutumia headphone za teknolojia ya Bluetooth  au zile zinazoweza kutumia tundu la lightning la kampuni ya Apple ambalo pia hutumiwa kuwekwa chaji.

Hata hivyo vifaa vya awali havitaacha kutumika kabisa na Apple inatarajiwa kuzindua kifaa ambacho kitamuwezesha mtu kutumia kuunganisha headphone na simu na kuendelea kuitumia.

Uzinduzi wa iPhone ulifanyika siku ya jana mjini San Francisco, Califonia.

Na imetoa aina mpya ya earphone zinazojulikana kama Airpods.

Sifa nyingine za simu hiyo;

Kitufe cha nyumbani sasa kinaweza kutofautisha uzito kinavyobonyezwa na kutoa mtikisiko. Kitufe hicho sasa hakiingii ndani ya simu.

Simu hizo zinaweza kuingizwa ndani ya maji ya kina cha 1m (3.2ft) kwa dakika 30 wakati mmoja bila kuharibika.

Aina kubwa ya iPhone 7 plus ina lensi mbili za kamera sehemu ya nyuma, ambayo inaimarisha uwezo wa kupiga picha.

Airpods zitagharimu £159. Pia zina uwezo wa kugundua zinapoingizwa masikioni. Hii inaziwezesha kusitisha uchezaji mziki zinapochomolewa maskioni.

Simu hizo zitaanza kuuzwa Septemba 16.


Wednesday, September 7, 2016

MUONEKANO MPYA WA RAY C.

Ray C katika mwonekano mpya.

Huo ndio mwonekano mpya wa mwanadada Ray C aliyekuwa akisumbuliwa na madawa ya kulevya.

Alituma picha yeye mwenyewe kwenye akaunti yake ya Instagram. Inasemekana pia Ray C ameondoka kwenye kituo cha sober kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam bila kutoa taarifa yoyote.


UTAFITI: VITAMIN D HUPUNGUZA PUMU.

Matumizi ya virutubisho vya Vitamin D pamoja na dawa za pumu hupunguza hatari ya shambulio la ugonjwa wa pumu.

Utafiti uliofanywa na watafiti wa Cochrane umebaini kwamba vinapunguza shambulio la wagonjwa wanaotumia steroids.

Lakini watafiti wanasema kuwa haijulikani iwapo inawasaidia wagonjwa walio na upungufu wa Vitamin D.

Wanasema utafiti zaidi unahitajika kabla ya kuwapa wagonjwa ushauri rasmi.

Walipendekeza kuzungumza na wauza dawa ili kupata ushauri kabla ya kutumia virutubisho vya Vitamin D.

Kiongozi wa watafiti hao Profesa Adrian Martineau anasema kuwa walibaini kwamba Vitamin D inapunguza makali ya Ugonjwa wa Asthma, bila kusababisha athari zozote.


MRISHO MPOTO: MR.BLUE NDIO MSANII BORA TANZANIA.

Mrisho Mpoto

Mwanamziki wa nyimbo za asili Tanzania, Mrisho Mpoto siku ya jana aliongea mkoani Tabora katika semina ya fursa ya Fiesta na kukiri kuwa Mr.Blue ndiye msanii bora Tanzania kwa sasa.

Mrisho aliyasema hayo maneno wakati anawaelimisha wakazi wa Tabora kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika nchi yetu.

"Nilikuwa sijui kama Mr.Blue ni yule kijana ambaye niliyekuwa namsikiaga enzi zile lakini Leo nimeuliza baada ya kuona akitumbuiza kwenye jukwaa la Fiesta nikaambiwa ni yeye" alisema Mpoto.

"Nabadilisha kauli zangu zote nilizowahi kusema nyuma, tena naangalia na Kamera kabisa na kusema Mr.Blue ndiye msanii bora Tanzania kwa sababu mpaka sasa ameweza kudumu kwenye tasnia hii ya mziki kwa muda mrefu bila kuacha" alimaliza kwa kusema hivyo.

Mr.Blue ni moja kati ya wasanii wachache waliotumbuiza Fiesta zote zilizoanza jijini Mwanza mpaka wiki hii ndani ya Tabora na Singida.


WANAODAIWA NHC KUPEWA SIKU SABA NA MAGUFULI.

Rais John Magufuli ametoa siku saba kwa taasisi zote za serikali zinazodaiwa malimbikizo ya kodi na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha zinalipa madeni yao, vinginevyo mali zao zitatolewa nje.

Dk. Magufuli amemtaka mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Nehemia Mchechu kutomuogopa mtu yeyote awe Rais, Waziri, CCM, Chadema au kiongozi yeyote wa serikali endapo hajalipa pango lake la nyumba, atolewe nje mali zake.

Pamoja na hayo mkuu wa nchi amewaahidi makazi wakazi 644 wa Magomeni kota wilaya ya Kinondoni kuwa ndani ya miezi miwili ujenzi wa nyumba za kisasa zitaanza katika eneo hilo na ndani ya mwaka mmoja zikishakamilika wakazi hao watakuwa wa kwanza kupatiwa nyumba hizo.

Akizungumza na wazee waliokuwa eneo hilo, Rais alisema tayari ameshatoa maagizo kwa taasisi zote za serikali zikiwemo Wizara zinazodaiwa na NHC kuhakikisha zinakamilisha madeni yao ndani ya siku saba.

"Wasipolipa nakuagiza Msechu watolee nje vitu vyao kama ulivyomtolea nje yule jamaa. Usiogope mtoe mtu yeyote asiyelipa pango. Lazima watu hawa wakulipe ili uweze kupata fedha za kuendeleza shirika hilo"alisema Magufuli.

"Nashangaa eti hawa wa serikalini wanashindwa kulipa pango la nyumba kwa NHC, lakini pesa za safari ya nje wanazo kila kukicha wanaomba vibali vya kusafiri na kupeana posho" alisema na kuongeza pia endapo shirika hilo litazitolea nje baadhi ya taasisi na Wizara za serikali kwa kushindwa kulipa kodi, itakuwa ni vyema kwakuwa sasa taasisi hizo zitaenda moja kwa moja Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kikamilifu.

Miongoni mwa taasisi zinazoongoza kudaiwa ni Ofisi ya Rais ml10, Wizara ya ujenzi na uchukuzi bilioni 2, Wizara ya Habari, tamaduni, Sanaa na michezo bilioni 1, Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto bilioni 1, Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ml 613, Tume ya haki za binadamu na utawala bora ml 360.


BEYONCE ASHAURIWA NA MADAKTARI KUPUMZISHA SAUTI.

Beyonce

Mwanamziki Beyonce amehairisha tamasha lake la New Jersey kwa jina la World Tour baada ya madaktari kumshauri kupumzisha sauti yake.

Msanii huyo ambaye alisherehekea siku yake ya 35 ya kuzaliwa siku ya jumapili alitoa taarifa  akisema tamasha hilo halitafanyika mnamo tarehe 7 Octoba.

Hata hivyo ataendelea na tamasha nyingine katika miji ya Los Angeles, Houston, New Orleans na Atlanta kama ilivyopangwa.

Ziara hiyo ambayo inalenga kuuza album yake mpya ya Lemonade ilianza mjini Miami mnamo tarehe 27 mwezi April.

Ilitarajiwa kukamilika Nashvile mnamo tarehe 2 mwezi Oktoba, lakini sasa inaonekana kwamba New Jersey itaandaa tamasha lake la mwisho


MWANAMKE AKAMATWA AKIUZA MABINTI.

Jeshi la polisi katika mkoa wa Mara linamshikiria Juritha Lucas (60) mkazi wa kijiji cha Masinki Wilaya ya Serengeti mkoani humo, kwa tuhuma ya kufanya biashara haramu ya binadamu kinyume cha sheria.

Kamanda wa polisi mkoani Mara, kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi Ramadhani Ng'azi alisema mwanamke huyo alikamatwa na polisi akiwa na mabinti watano wenye umri kati ya miaka 15 na 23 alokuwa anataka kuwauza.

Kamanda Ng'azi alisema mabinti hao ni wakazi wa kijiji cha Muruvyagiza, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, ambako ndiko mwanamke huyo aliwatoa na kuwasafirisha hadi katika kijiji cha Masinki Wilayani Serengeti, kwa nia ya kuwauza kwa kuwaozesha kwa wanaume kwa bei kati ya 150,000 hadi 300,000 kila mmoja kulingana na umri, uzuri na tabia ya binti husika.

Polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema kuhusu biashara hiyo, waliweka mtego na ndipo Septemba 4 mwaka huu walimkamata mwanamke huyo na kumhoji na akakiri kuwachukua mabinti hao kutoka mkoani Kagera kwa ajili ya kuwauza.

Jitihada zinafanyika ili kuwasiliana na wazazi wa mabinti hao ili kuwachukua.

Kamanda Ng'azi hakuwataja majina kwa ajili ya usalama, lakini walisema wanaendelea na uchunguzi wa kina na kuwa baada ya upelelezi kukamilika watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma ya kufanya biashara ya binadamu kinyume cha sheria.