Maandalizi ya maziko ya Spika mstaafu na mwanasiasa mkongwe wilayani Urambo mkoani Tabora, Samuel Sitta yanaendelea huku ndugu na jamaa wa karibu wakiendelea kuwasili wilayani humo.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu mjini Urambo jana, mdogo wake Peter Sitta alisema maandalizi yanaendelea huku wakiendelea kusubiri taarifa za ratiba kutoka kwa Kamati ya Bunge iliyoundwa kuratibu.
Peter alisema awali alipokea taarifa za ambazo zilikuwa zikieleza kuwa hali ya Spika mstaafu si nzuri baada ya kupigiwa simu saa 11:50 alfajiri, na baada ya muda kidogo alipigiwa simu na kufahamishwa kuhusu msiba kutoka huko kwenye matibabu nchini Ujerumani.
Alifafanua kuwa alishtuka sana kwani ni siku chache tu alikuwa anawasiliana naye wakijuliana hali kwani hata yeye hali yake siyo nzuri.
“Nimestushwa sana kwani nimeongea naye kwenye simu akanijulisha afya yake na kusema anaendelea vizuri na matibabu na yeye Samuel alimuuliza kuhusiana na afya yangu kwani hata mimi naumwa pia,” alieleza Peter.
Alieleza kabla ya kifo chake walizungumza kwenye simu baada ya ndugu aliyekuwa akimuuguza kumwambia waongee na ndipo aligundua hali siyo nzuri kwani alikuwa anaongea kwa taabu mno.
Alieleza kuwa kutokana na mazungumzo yale aligundua hali ya kaka yake si nzuri.
Akizungumzia maandalizi ya maziko, alisema hadi sasa haijafahamika kwani kuna Kamati ya Bunge iliyoundwa ambayo imekuwa ikiratibu maandalizi yote na baada ya mwili kuwasili kutokana Ujerumani ndipo kutakuwa na taarifa sahihi za mazishi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi alilieleza gazeti hili kuwa msiba huo, umemshitusha na hakutarajia.
Alisema amepokea kwa masikitiko makubwa kwani chama kimepoteza shujaa wa kisiasa mkoani Tabora na nchi kwa ujumla. Katibu wa CCM Wilaya ya Urambo, Innocent Nanzabar alisema Mkoa wa Tabora na wilaya ya Urambo, wamepoteza mtu muhimu kwao.
Alisema Sitta alifahamika kama ‘chuma cha pua’ hivyo kuzoeleka kwake na jamii itawachukua muda kumsahau. Alisema atakumbukwa kwa mengi kwa jinsi alivyokuwa mpigania haki, mchukia rushwa na kamwe hakupenda uonevu kwa wanyonge na serikali kwa ujumla.
Mama mzazi wa Sitta, Hajjat Zuwena Saidi Fundikira akizungumza kwa masikitiko huku akibubujikwa na machozi, alisema hana cha kusema zaidi ya kulia.
“Nilipokea taarifa hizi kutoka kwa mwanangu Peter John Sitta baada ya kufika nyumbani huku akilia na baada ya kunyamaza ndipo alinieleza kuwa kuna msiba,” alisema na kuongeza kuwa kamwe hatamsahau mtoto wake kwani bila ya marehemu yeye asingeijua ibada ya hija kwani alimpenda katika maisha yake.
No comments:
Post a Comment