MBWANA SAMATTA |
Nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta anatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam kesho Jumatano kujiunga na kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe mwishoni mwa wiki.
Kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii za jana, Samatta aliondokana jana Genk, Ubelgiji kupitia Dubai kabla ya kutua jijini Dar es Salaam kesho.
Samatta ameendelea kuonesha umuhimu wa kuichezea Taifa Stars kwa kuitikia mwito wa kocha Charles Boniface Mkwasa licha ya kuwa na majukumu mazito katika klabu yake. Klabu yake hiyo mbali na kushiriki Ligi Kuu ya Ubelgij, pia inashiriki katika Ligi ya Ulaya.
Wachezaji 24 walioitwa na Mkwasa kwa ajili ya mchezo huo wa Novemba 13 mjini Harare, walitarajia kuingia kambini jana.
Wachezaji wa Taifa Stars walioitwa na Mkwasa ni makipa;Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga, Said Kipao wa JKT Ruvu na Aishi Manula wa Azam FC.
Mabeki; Erasto Nyoni, David Mwantika wa Azam FC, Michael Aidan wa JKT Ruvu, Mwinyi Hajji, Vincent Andrew wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC na James Josephat wa Prisons.
Viungo wa kati: Himid Mao wa Azam FC, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Jonas Mkude na Muzamil Yassin wa Simba SC, wakati viungo wa pembeni ni Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting, Shizza Kichuya, Jamal Mnyate wa Simba SC na Simon Msuva wa Yanga.
Washambuliaji ni Ibrahim Ajib wa Simba SC, John Bocco wa Azam FC, Elius Maguli wa Oman Club, Thomas Ulimwengu aliyemaliza mkataba wake TP Mazembe ya DRC na kuondoka mwezi uliopita, Omar Mponda wa Ndanda FC na Nahodha Mbwana Samatta wa K.R.C Genk ya Ubelgiji.
No comments:
Post a Comment