Mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya ombi la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) la kuongeza bei ya nishati hiyo kwa wastani wa asilimia zaidi ya 18.9 ifikapo mwaka 2017, unatarajia kuanza.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeeleza kuwa Oktoba 4, mamlaka hiyo ilipokea ombi la mabadiliko ya bei ya umeme, hivyo unaandaliwa mkakati wa kukusanya maoni ya wadau wa nishati hiyo.
“Mikutano ya ukusanyaji maoni kuhusu bei inayopendekezwa na Tanesco itaanza Novemba 16 katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma na kwa Dar es Salaam ni Novemba 23,” inaeleza taarifa hiyo.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miezi saba tangu kutangazwa kwa bei mpya ya umeme iliyokuwa na punguzo la asilimia 1.5 hadi 2.4 sanjali na kuondoa tozo ya kuunganishiwa umeme ya Sh5,000 na gharama ya huduma kwa kila mwezi ambayo ilikuwa na Sh5,520.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema shirika hilo limefanya tathmini na kujiridhisha kuwa hakuna hasara itakayopatikana endapo bei hiyo itatumika.
No comments:
Post a Comment