Tuesday, November 8, 2016

MANENO MATATU YA MWISHO YA SITTA KABLA YA KIFO.

MAREHEMU SAMWEL SITTA
Kabla ya kifo chake Spika wa Bunge mstaafu, Samuel Sitta alisema maneno matatu ya Kiingereza, “that is life” (hayo ndiyo maisha).
Sitta alitamka maneno hayo baada ya kuambiwa na daktari wake kwamba hawezi kupona ugonjwa unaomsumbua.
Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, Benjamin Sitta ambaye ni mtoto wa Sitta alisema baada ya kuzungumza maneno hayo baba yake alifariki dunia.
Alisema baada ya kuelezwa ukweli huo na daktari, baba yake alikubali kwamba huo ndiyo mwisho wa maisha yake hapa duniani.
“Tumepoteza baba na kiongozi ambaye tulimtegemea kwa ushauri wa masuala mbalimbali, tutafuata yale aliyokuwa akituelekeza,” alisema Benjamin ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni.
Sitta alifariki dunia saa 10.50 alfajiri kwa saa za Tanzania  wakati akipatiwa matibabu ya saratani ya tezi dume katika Hospitali ya Technical University of Munuch nchini Ujerumani.
Mwezi uliopita mbunge huyo wa zamani wa Urambo Mashariki alirejea nchini akitokea Ujerumani alikokuwa akitibiwa, lakini wiki iliyopita alienda tena kwa ajili ya matibabu zaidi.
Benjamin alisema marehemu atazikwa wilayani Urambo mkoani Tabora, lakini ratiba ya mazishi ingetolewa na ofisi ya Bunge ambayo inaratibu msiba huo.
“Kwa sasa hatujui mwili utawasili nchini lini, utaagwa lini na atazikwa lini ila tunachofahamu ni kuwa atazikwa Urambo,” alisema.
Benjamin alisema masuala mengine yanayohusu familia hiyo yatazungumzwa na mama yake, Magareth Sitta ambaye bado yuko Ujerumani. “Mambo mengine naomba niyaache yatazungumzwa na mama baada ya kurudi nchini, unajua sasa yeye ndiyo nguzo ya familia, hivyo ni vizuri tukamsubiri yeye,” alisema.
Nyumbani kwa marehemu
Watu walikusanyika nyumbani kwa marehemu  Masaki jijini Dar es Salaam tangu saa 2.30 asubuhi jana baada ya taarifa za kifo hicho kusambaa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Miongoni mwa waliofika mapema ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida ambaye alimwelezea Sitta kuwa atakumbukwa kwa mchango mkubwa katika Serikali na chama hicho.
“Sitta alikuwa kiongozi mwadilifu na aliyesimamia haki katika Serikali na CCM, ndiyo maana wakati wa uhai alikuwa mtu wa watu,” alisema Madabida.
Alisema ukiondoa nyadhifa nyingine za uwaziri, uspika na uenyekiti wa Bunge la Katiba, Sitta atakumbukwa kwa kuongoza vizuri Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Aden Rage alisema mafanikio yake katika siasa ulikuwa ni mchango mkubwa alioupata kutoka kwa Sitta.
“Ni pigo kubwa kuondokea na mtu wa aina ya Sitta, busara zake tulizitegemea kupata ushauri, maneno yake yataendelea kuishi vichwani mwetu,” alisema.
Akiungana na Rage, mdogo wa marehemu, Paulo Sitta alisema kaka yake alikuwa mlezi wa familia na ndugu zake kwa ujumla.
“Familia na ndugu zake tumepata pigo kwa kuwa alikuwa mlezi wetu,” alisema.
 Rais Magufuli atuma salamu
Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai kufuatia kifo cha Sitta.
Rais Magufuli alisema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Sitta na kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali,” alisema.
Rais alitoa pole kwa mke wa marehemu, Magareth Sitta ambaye ni mbunge wa Jimbo la Urambo, familia, wabunge, wananchi wa Urambo na wote walioguswa na msiba huo.
Salamu za CCM
Katika taarifa yake, CCM ilisema imepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa za kifo cha Sitta ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za utumishi katika chama na Serikali.
Akiwasilisha salamu za rambirambi za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa Spika Ndugai, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema Sitta alikuwa ni kiongozi mchapakazi, mwadilifu na aliyejitambulisha kwa utendaji wenye kufuata falsafa yake ya “kasi na viwango”.

No comments: