Tuesday, November 8, 2016

MAMBA MLA WATU AUAWA.


Mamba mla watu aliyekuwa tishio kwa wakazi wa Kijiji cha Kakobe katika Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ameuawa na wananchi na kuchunwa ngozi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kazunzu, Timotheo Sengerema amesema kuuawa kwa mamba huyo kumewaondolea hofu wakazi hao waliolazimika kusitisha shughuli za uvuvi ndani ya ziwa hilo wakihofia kuuawa na kuliwa.
“Kabla ya kunaswa na kuuawa juzi, mamba huyo alikuwa amewauwa wavuvi watatu walipokuwa kwenye shughuli zao za uvuvi,” amesema Sengerema.
Amesema kazi ya kumtega na kumnasa mamba huyo ilitekelezwa na mmoja wao mwenye ujuzi wa kazi hiyo, Lucas Dambaya kwa ahadi ya kulipwa Sh1 milioni zilizochangwa na wanakiji hao.
“Kazi ya kumtega na kumnasa mamba huyo ambaye wanakijiji  walimchuna ngozi kabla ya kuukabidhi mzoga wake kwa uongozi wa kata ilichukua siku mbili,” amesema Sengerema.
Akizungumza baada ya kumnasa mamba huyo, Dambaya amesema ataendelea kuweka mitego kuwanasa mamba wengine ambao  bado wako kwenye mwalo wa kijiji hicho na kuwataka wakazi hao kuchukua tahadhari wanapofanya shughuli zao ziwani humo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, George Mambile amesema kwa kipindi cha miezi mitatu, wakazi hao walikuwa wakiishi kwa hofu ya kudakwa na mamba huyo mla watu.
Aliushukuru uongozi wa kata kwa kusaidia juhudi za kumkamata na kumuua mamba huyo.

No comments: